RAHA UTAMU

Jumanne, 10 Juni 2014

Endelea kusoma hadithi hizo za Shigongo

HII ni historia ya kweli ya maisha yangu, kuna baadhi ya watu nakutana nao wananiuliza kama hii ni hadithi kama ambazo nimekuwa nikiandika magazetini. Nataka nisisitize kwamba hii ni historia ya kweli kabisa ya maisha yangu, najaribu kuyapitia maisha yangu ya nyuma na kuwaandikia watu kule nilikopitia.
Lengo langu ni nini? Kumtia moyo mtu aliyevunjika moyo na kumfanya aamini inawezekana kufanikiwa hata kama unatoka familia masikini. Nayasema haya kwa sababu wako watu leo hii wamekata tamaa kabisa na kuamini kwamba watu fulani wanaweza kufanya vizuri maishani na si wao, uongo mkubwa na mbinu ya shetani kuwafanya watu waendelee kuteseka.
Yeyote anayesoma historia yangu ni lazima hata kama yuko katika hali ngumu kiasi gani,  aamini kwamba inawezekana, kama iliwezekana kwangu inashindikanaje kwa mtu mwingine? Inuka hapo ulipo, amini akili yako, fanya jambo jema hata kama ni dogo kiasi gani, ukilifanya kwa muda mrefu hatimaye jambo kubwa litakutokea, huu kwangu ni ukweli uliothibitishwa na mimi mwenyewe.
Lengo si kujitapa bali kuwaonesha watu jinsi Mungu anavyoweza kumbariki mtu na ninajua kutoka ndani ya moyo wangu ya kwamba Mungu alininyanyua kwa kusudi moja tu; yeyote aliyekata tamaa atakaponiangalia mimi apate tumaini na kuamini kwamba kumbe inawezekana.
Endelea mwenyewe...
Kitu kimoja naomba niseme hapa ni kwamba kipindi chote wakati namuuguza kaka yangu, baba, mama na ndugu zangu wote walikuwepo jijini Dar es Salaam, wakiungana nami kwa kila jambo, familia yetu ilikuwa ya umoja kupindukia hilo ndilo jambo Mungu alilotujalia. Hivyo baada ya msiba, taarifa zilishasambaa kwa watu wote wa karibu.
Msiba huu wa kaka uliniumiza mno sikuwahi kuumia kiasi hicho maishani mwangu pengine niseme ulinifanya nikumbuke mema yote ya nyuma aliyonifanyia, aliipenda sana familia alikuwa tayari kuteseka kwa kitu kidogo alichopata lakini aifanye familia yake iishi, hakika alikuwa mtu muhimu mno, ni huyu ndiye aliyenipa mtaji ambao umenifikisha hapa nilipo leo, Mungu amlaze mahali pema peponi.
Ni hapo ndipo msemo huu wa Kifo kisikie kwa jirani yako kikija kwako kinauma mno uliingia ndani ya kichwa changu, nikauamini kwa jinsi nilivyoumia, pamoja na yote nilikumbuka maneno ya baba kwamba huwa wanaume hawalii hivyo nilijikaza kiume.
Watu walipofika nyumbani kunipa pole tuliongea mengi lakini ndani ya moyo wangu nilikuwa na maumivu makali mno, yalipozidi sana niliingia chumba na kulia. Ni mke wangu pekee aliyefahamu jambo hili na kunibembeleza akinipa moyo na kunifariji na baada ya kutulia nilinawa uso nikavalia miwani yangu ya rangi nyeusi kisha kutoka nje kuendelea na mazungumzo na wageni wetu.
Mipango ya mazishi ikaanza, taarifa zikapelekwa Nyakato ambako ndiko nyumbani kwetu. Mwenyekiti wa mtaa, mzee Machota, vijana wote wa Mecco akina Matiku, Isdori na wengineo wengi waliungana nasi mara baada ya kuwasili mjini Mwanza.
Ni kama vile msiba ulianza upya, walikuwepo ndugu wengi mno kutufariji na kuomboleza pamoja nasi, naikumbuka kwaya moja ya AICC Neema. Kwaya hii iliimba mno nyimbo za kututia nguvu, uchungu ukapungua kidogo na utaratibu wa mazishi ukaanza.
Watu walikuwa wengi kupindukia, ni hapo ndipo nilipogundua upendo wa watu wa Mwanza, nikagundua kwamba watu hao walinipenda kupita kiasi na walinithamini na kunipa nguvu kwa mambo yote.
Baada ya ibada kwisha tulianza safari ya kwenda makaburini, nakumbuka yalikuwa makaburi ya Kangae, hapo ndipo alipozikwa kaka yangu mpendwa, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina. Hakika nitamkumbuka daima kwa wema wa ajali aliniotendea.
Wakati ibada inaendelea nikatupa macho yangu pembeni  na kushuhudia makaburi mengi madogo madogo yakiwa hapo,  akili yangu ikarejea nyuma na kumkumbuka dada yangu mpendwa Jesca ambaye alikufa miaka mingi iliyopita, huyu alizikwa na kaburi lake kupotea kwa sababu ya umasikini mkubwa tuliokuwa nao mimi na familia yangu, hivyo mahali alipozikwa wakaja watu wenye fedha na kununua eneo lile kisha kuchimba na kujenga nyumba za kifahari, kitu kilichopoteza kabisa kumbukumbu yake, moyo wangu ukaniuma tena.
Nikaangua kilio bila kujali tena kwamba mimi kama kaka mkubwa wa familia nilitakiwa kujikaza, hakika uvumilivu wangu ulishakwisha, nikajikuta nikimwaga machozi mpaka rafiki zangu waliokuwa wamenizunguka wakanisihi na kunibembeleza kwamba sikutakiwa kufanya hivyo hata kama nilikuwa katika maumivu makali kiasi gani. Nadhani ni kwa sababu hawakujua nini kinanisumbua ndani ya kichwa changu.
Wakati ibada inaendelea  mimi niliwaza jambo moja tu, kununua shamba ambalo niliamini lingeweza kuweka kumbukumbu nzuri kwa  kizazi kijacho, watoto na wajukuu wa watoto wetu, nikaapa kununua shamba kubwa  ili jambo lililokuwa limejitokeza kwa Jesca lisije likajirudia tena katika familia yangu.
Nikatamani familia yangu iwe na shamba kwa ajili ya kuzika ili kuweka  historia kwa kizazi kijacho na kitakachodumu siku zote, ibada ikawa imekwisha  lakini ndani  ya kichwa changu nikiwa na wazo moja tu, kununua shamba. Sikutaka yaliyotokea kwa marehemu dada yangu Jesca yatokee tena katika familia yangu hivyo ndivyo nilivyojiapiza.
Ibada ikawa imekwisha  na watu wakaanza kutembea kurejea tena nyumbani kuendelea na shughuli nyingine nakumbuka nilipiga hatua moja na niliponyanyua kupiga ya pili, nikageuka nyuma na kuangalia kaburi la kaka yangu, nikalia kwa uchungu, tulikuwa tukiondoka na kumwacha peke yake tena sehemu ambayo hapakuwa na mtu yeyote isipokuwa  yeye tu.
Uchungu ulizidi zaidi pale nilipomwangalia mtoto mdogo wa kiume wa kaka yangu ambaye aliachwa na mama yake. Hapo ndipo nilipojua nini maana ya maisha lakini nikamuahidi Mungu kufanya kila kinachowezekana kumpa mtoto huyo furaha maisha yake yote nikichukua jukumu lote la kumlea na kumtunza vyema kama ambavyo baba yake alifanya kwangu.
Nikalia tena lakini nikatamka ndani ya  moyo wangu kwamba hatimaye shujaa alikuwa amepumzika baada ya kuteseka kwa muda mrefu, kufa kwa kaka yangu kukanifanya mimi nichukue mikoba yote aliyokuwa nayo, jukumu la kuitunza familia likarejea kwangu kwa mila na desturi za Kisukuma mwanaume hata kama ni mdogo kiasi gani aliitwa kaka, hivyo ndivyo ilivyo.
Tukarejea nyumbani na kuendelea kuomboleza, watu bado wakiwa nasi, wakiendelea kutufariji na kututaka badala ya kuendelea kuhuzunika sasa tufurahi na kumshukuru Mungu kwani ndiye anayepanga yote yatokee.
Siku zikaendelea kusonga mbele, mpaka siku ya tatu, watu wengi wakiwa bado wapo nyumbani kwetu kutufariji, wanakwaya nao bado walikuwepo, hawakuchoka kuwa nasi. Ninawashukuru sana na Mungu aendelee kuwabariki siku zote.
Baadaye watu walianza kutawanyika kurejea makwao baada ya kukaa nasi kwa kipindi kirefu, sasa ulikuwa wakati wa wao kuendelea na shughuli zao na kutuacha sisi tufanye yetu kama familia. Hapa ni kama vile uchungu ulirejea tena upya lakini kwa sababu ya majukumu hatukuwa na sababu ya kuendelea kuwazuia, tukawashukuru na kuwatakia baraka zote huku wakiahidi kuendelea kuwa nasi  katika maombi.
Mimi pia na familia yangu baada ya kuhakikisha kila kitu kimekwenda sawa tulianza mipango ya kurejea jijini Dar es Salaam ili kuendelea na shughuli nyingine.
Usikose kufuatilia katika Gazeti la Ijumaa Wikienda wiki ijayo

HADITHI YA KUSISIMUA AISEEEEEE

BAADA ya gari kusimama pembeni na kutakiwa watawa wote waliokuwa kwenye gari kushuka, Sister Anna alipinga kitendo cha kushushwa kwenye gari.

“Jamani hivi watumishi wa Mungu wanaweza kuwa wauaji?”

“Sister hili ni agizo la mheshimiwa rais kuwakagua wote wanaopita njia hii, hasa baada ya mtuhumiwa kuonekana bonde la Kizugo. Sehemu yote ya mapori kumetanda wanajeshi kwa hiyo kila atakapokimbilia lazima ashikwe.”

“Sasa sisi tunahusika vipi na mtu huyo?”

“Sister we wasiwasi wako…
Added by GLOBAL on June 9, 2014 at 8:00am — 9 Comments

A Saint and a Ghost (Mtakatifu na Mzimu) - 94

Mfululizo wa matukio ya ajabu unaendelea kuyatawala maisha ya msichana mdogo, ambaye maisha yake yametawaliwa na usiri mkubwa. Kwa kumtazama, huwezi kugundua chochote kilichojificha nyuma ya maisha yake kwani uzuri wa sura yake, upole na urembo wake, vinamfanya aonekane hana hatia machoni mwa watu.
Hata hivyo, kuna siri kubwa iliyojificha nyuma ya maisha yake ambayo ameishi nayo kwa kipindi kirefu. Ukweli ambao hakuna anayeujua ni kwamba msichana…
Added by GLOBAL on June 9, 2014 at 7:00am — 7 Comments

True Memories Of My Life [Kumbukumbu za Kweli za Maisha Ya Shigongo] - 82

HII ni historia ya kweli ya maisha yangu, kuna baadhi ya watu nakutana nao wananiuliza kama hii ni hadithi kama ambazo nimekuwa nikiandika magazetini. Nataka nisisitize kwamba hii ni historia ya kweli kabisa ya maisha yangu, najaribu kuyapitia maisha yangu ya nyuma na kuwaandikia watu kule nilikopitia.
Lengo langu ni nini? Kumtia moyo mtu aliyevunjika moyo na kumfanya aamini inawezekana kufanikiwa hata kama unatoka familia masikini. Nayasema haya kwa sababu…
Added by GLOBAL on June 9, 2014 at 6:30am — 1 Comment